JINSI YA KUJIBU MASWALI YA FASIHI
UTANGULIZI
Kijitabu hiki ni mwongozo wa namna ya kujibu
maswali ya tamthiliya, riwaya na ushairi. Mada hii imekuwa ngumu na yenye
changamoto kubwa, hapana shaka kuwa kijitabu hiki kitarahisisha ugumu huo.
Katika mtihani wa mwisho wa kidato cha nne, maswali yahusuyo tamthiliya, riwaya
na ushairi yanapatikana sehemu ya mwisho yaani sehemu E. Swali la 12 huhusu
ushairi. Swali la 13 linahusu riwaya. Swali la 14 linatazamia tamthiliya.
Utatakiwa kuchagua maswali mawili unayoyaweza. Huenda ukachagua swali la riwaya
na tamthiliya au riwaya na ushairi lakini huwezi kufanya swali la riwaya
tamthiliya na ushairi yote kwa pamoja, lazima uchague maswali mawili na moja
litabaki. Swali moja huwa na alama 15% hivyo ukiyafanya vyema utapata alama
30%... alama hizi ni nyingi na zinaweza kukuvusha hatua moja kwenda nyingine
hivyo ni vyema kuzitafuta. Mwanafunzi atakaye kisoma kijitabu hiki ataweza
kujibu maswali ya tamthiliya, ushairi na riwaya. Kukisoma kitabu hiki ni
kumiliki alama 30% za mtihani wa mwisho wa kidato cha nne hata kabla ya
kuufanya mtihani wenyewe!
SEHEMU YA KWANZA; USHAIRI
Kama wasemavyo Mlokozi na Kahigi (1982;25),
‘ushairi ni sanaa inayopambanuliwa kwa mpangilio maalumu wa fasaha na wenye
muwala, kwa lugha ya picha, sitiari au ishara katika usemi, maandishi au
mahadhi ya wimbo ili kuleta wazo au mawazo, kufunza au kueleza tukio au hisia
fulani kuhusu maisha au mazingira ya binadamu kwa njia inayogusa moyo.’ Hivyo
basi tunaweza kusema kuwa, ushairi ni mpangilio maalumu wa maneno yenye lugha
ya picha na ya mkato wenye lengo la kufunza jambo fulani.
SEHEMU KUU KATIKA INSHA YA USHAIRI
i.Utangulizi
ii.Kiini
iii.Hitimisho
UTANGULIZI
Katika utangulizi ni vyema kuzingatia mambo
manne muhimu;
i.Toa maana ya neno uliloulizwa
ii.Kubali au kataa kauli iliyopo katika swali
iii.Taja majina ya vitabu utakavyovitumia
katika kujibu swali lako. (vitabu viwe viwili na majina yaandikwe kwa herufi
kubwa) iv.Tambulisha kitabu unachoanza kujibu swali KIINI Kiini hupaswa kuwa na
hoja tatu, ama kwa wale wenye utajiri wa hoja na kasi ya kuandika basi ukingo
wao uwe hoja nne kwa kila kitabu. Kila hoja inatakiwa iwe na mambo matano
muhimu;
i.
Hoja
yenyewe
ii.
Jina la
shairi linalothibitisha hoja hiyo
iii.
Maelezo
ya hoja hiyo
iv.
Nukuu ya shairi. (nukuu itolewe na yule aliyekariri mistari au beti za shairi
husika, la, hujakariri basi usidanganye ukapoteza alama hata za ule ukweli
ulioueleza)
iv.
Onesha
uhusiano wa kile ulichokisema na jamii yako. Kwa maana fasihi ni zao la jamii
na kujaribu kuitenga na jamii ni kukaanga mawe kwa matarajio ya kula maini!!
HOJA YA KUKARIBISHA KITABU CHA PILI
Hii ndio hutoa taarifa kuwa umehama kitabu
cha kwanza na sasa unaingia kitabu kingine, mara nyingi hujengwa kwa maneno
kama, sambamba na hayo, fanaka na hayo, kwa kuachana na hayo, n.k nilipokuwa
mwanafunzi kwa ngazi uliyopo nilipenda kutumia, sambamba na hayo… sina sababu
ya uchaguzi huo ila waweza tumia neno lolote kati ya hayo yaliyoorodheshwa.
HITIMISHO
Huu nu muhtasari wa kile ulichokieleza.
Andika hitimisho lako kwa ufupi tu, lugha fasaha yenye kueleweka na epuka
porojo na mizunguko isiyokuwa na maana. Sio vigumu… ni rahisi sana, mfano
ufuatao unaelezea zaidi.
Swali la necta mwaka 2013 “Mshairi siku zote
hukemea uonevu katika jamii.” Thibitisha kauli hii kwa kutoa hoja tatu kutoka
katika kila diwani kati ya diwani mbili ulizosoma.
JIBU
Uonevu ni kumfanyia mtu jambo la
dhuluma au mateso. Ni kweli kabisa kuwa mshairi siku zote hukemea uonevu katika
jamii. Kauli hiyo yaweza kuthibitishwa kwa kutumia diwani mbili, MASHAIRI YA
CHEKECHEKA kilichotungwa na Theobard Mvungi na WASAKATONGE chake Mohammed
Seif Khatib. Kwa kuanza na MASHAIRI YA
CHEKACHEKA tunaona kuwa,
Mshairi
anakemea usaliti. Suala hili linaonekana katika shairi la MASHAIRI YA NGULU.
Mshairi anaikemea serikali kwa kushindwa kupeleka huduma za kijamii vijijini na
hivyo kufanya maisha ya huko yawe ya tabu. Mshairi anasema,
‘Ngulu kule kijijini, chanzo cha huyu malenga,
Ngulu katika diwani, kijiji kisichoringa,
Ngulu taringia nini, ni mengi yamenizinga.’
Ni
kweli kuwa wanachi hao wamesalitiwa hata hawawezi kuringa. Hata katika jamii
yetu vipo vijiji mfano wa Ngulu, vijiji ambavyo vimenyimwa huduma muhimu kama
umeme na maji ni vyema visaidiwe.
Mshairi
anakemea matabaka. Suala hili linaonekana katika shairi la UTU UMEKUWA KIMA.
Mshairi amejadili kwa kina na kuonesha jinsi ambavyo tabaka tawala
linavyowanyanyasa wasionacho. Mshairi anasema,
‘Yenye miiba ya mkonge,
Kunyang’anyana
matonge,
Mwenye
nguvu ndiye mtu.’
Mshairi anatamani kuiona jamii ambayo haina
matabaka. Hata katika jamii yetu, tabaka la chini linanyanyaswa na tabaka
tawala, ni vyema matabaka yakaondolewa.
Mshairi
anakemea uongozi mbaya. Suala hili linaonekana katika shairi la TUAMBAE
UKASUKU. Mshairi anawashauri wasanii wote waungane ili wakemee uongozi mbaya.
Mshairi anasema,
‘Beti kali tuzitunge, ziwakate wahujumu,
Zikemee hata wabunge, wazembe tuwahukumu,
Wabunge waote meno, wasivirambe viatu.’
uongozi mbaya ni chanzo cha maovu yote. Hata katika jamii
yetu uongozi mbaya upo, athari zake ni kuongezeka kwa umasikini, ni vyema
uongozi mbaya uondolewe.
Sambamba na hayo,
kwa kutumia diwani ya WASAKATONGE, tunaona kuwa,
Mshairi anakemea rushwa. Suala hili
linaonekana katika shairi la MVUJA JASHO. Mtu wa chini ananyanyaswa kwa kuombwa
rushwa katika kila jambo na kumcheleweshea maendeleo. Mshairi anasema,
‘Rushwa imezagaa,
Uozo
ulojaa,
Hakuna
manufaa.’
wananchi hawapati manufaa ya jasho lao kwa
sababu ya rushwa. Katika jamii yetu rushwa ipo na imeendelea kuwa adui wa haki,
ni wakati sasa wa kuungana pamoja na kuipinga rushwa.
Mshairi
anakemea ukeketaji wa mwanamke. Suala hili linaonekana katika shairi la TOHARA.
Mshairi anashauri kuepukana na ngariba kwani wao ndio vinara wa ukeketaji
wanawake. Mshairi anasema,
‘Epuka hao ngariba, wajuaji,
Hufika navyo viroba, wachinjaji,
kumbuka hawana tiba, wauaji…’
Mshairi hakubaliani kabisa na suala la
ukeketaji wa mwanamke. Katika jamii yetu ukeketaji wa mwanamke bado unaendelea,
suala hili limesababisha vifo vya wanawake wengi. Ni wakati sasa jamii
inatakiwa kuachana na mila hii mbaya.
Mshairi
anakemea manyanyaso wanayofanyiwa wanachi wa kawaida. Suala hili linaonekana
katika shairi la KOSA? Wananchi wananyanyaswa bila kosa lolote la msingi, mshairi
anasema,
‘msitunyanyase,
sio watwana,
watu wa mana,
tuloungana…’
wananchi wananyanyaswa kwa sababu ya kudai
haki zao. Jambo hili halikubaliki. Hata katika jamii yetu manyanyaso yapo ya
kila aina, ni vyema wananchi wakaheshimiwa na kuacha kunyanyaswa hasa pale
wanapojitokeza kudai haki zao.
Hivyo ndivyo mshairi alivyokemea uonevu katika
jamii. Mambo yanayokemewa na mshairi yakifanyiwa kazi kwa kuyaondoa yale
yasiyofaa, jamii mpya yenye misingi ya ubinadamu itapatikana na kuifanya Dunia
iwe mahali salama.
SEHEMU
YA PILI; RIWAYA NA TAMTHILIYA
Maswali ya riwaya na tamthiliya hujibiwa kwa
muundo wa aina moja. Hakikisha kwamba kabla hujajibu swali la riwaya au
tamthiliya uwe umelielewa, lazima uelewe swali linataka nini, baadaye uwe na
uelewa wa jinsi ya kulijibu swali hilo. Insha yako ya riwaya au tamthiliya
inatakiwa iwe na sehemu sita muhimu kama zifuatazo; Utangulizi Mambo muhimu ya
kuzingatia katika kipengele hiki ni;
Toa maana ya kitu unachotakiwa kujibu
Kubali au kataa ukweli wa kauli iliyotolewa
Toa ushahidi wa kukubali au kukataa kwa kutumia vitabu viwili
Majina ya vitabu yaandikwe kwa herufi kubwa na yaandikwapo kwa herufi ndogo
basi yapigiwe msitari.
Aya ya
kutambulisha kitabu cha kwanza
Toa
hoja za kitabu cha kwanza
Zingatia kuwa kila aya angalau iwe na mistari mitano tu. Ikizidi basi iwe saba
au nane.
Waweza tumia aya tatu au nne kwa kitabu kimoja
Epuka kutoa maelezo mengi kupita kiasi na lugha za mizunguko
Aya ya kukaribisha kitabu
cha pili. Maneno yatumiwayo ni, pamoja na hayo, sambamba na hayo, vilevile n.k
Hoja za kitabu cha pili Hitimisho Kwa vile fasihi ni zao la jamii basi haina
budi majibu yako ukayahusisha na jamii.
Mfano
wa kwanza; swali la riwaya Swali la necta mwaka 2013 “Fasihi ni chuo cha
kufundisha maisha kwa jamii husika. “Jadili ukweli wa kauli hii kwa kutoa hoja
tatu kwa kila riwaya kati ya riwaya mbili ulizosoma.
JIBU
Fasihi ni
sanaa ambayo hutumia lugha kufikisha ujumbe wake. Ni kweli kabisa kuwa, fasihi
ni chuo cha kufundisha maisha kwa jamii husika. Kauli hii yaweza kuthibitishwa
kwa kutumia riwaya mbili, WATOTO WA MAMAN’TILIE yake Emmanuel Mbogo na TAKADINI
iliyotungwa na Ben J Hanson. Kwa kuanza na
riwaya ya WATOTO WA MAMAN’TILIE, kauli hii inathibitishwa,
Fasihi
inatufundisha kuwa ulevi si jambo jema. Mzee Lomolomo ni mlevi mtiifu, pesa
yake yote iliishia kwenye pombe. Ulevi ndio unamfanya mzee huyu ashindwe
kusomesha watoto wake na kujikuta wakifukuzwa shule. Madhara ya ulevi
yanaonekana zaidi pale anapokunywa pombe zilizokwesha muda wake na
kumsababishia kifo. Katika jamii yetu ulevi umekithiri, watu wanaokunywa pombe
muda wa kazi ni mfano tosha, ulevi utokomezwe kwani ni chanzo cha umasikini.
Fasihi
inatufundisha kuwa watoto wasifukuzwe shule kwa kukosa ada. Watoto Zita, Pita
na Musa wanafukuzwa shule kwa kukosa ada, kufukuzwa kwao kunawafanya wakose
mwelekeo, Musa na Pita wanajiingiza katika biashara ya madawa ya kulevya na
kuwafanya wakamatwe na polisi. Katika jamii yetu mambo yamerekebishwa kiasi
kuwafanya watu wote wapate elimu bora bila kulipia kutoka darasa la kwanza
mpaka kidato cha nne. Ni vyema pia huduma mbalimbali zikiboreshwa zaidi ili
kutoa elimu bora.
Fasihi
inatufundisha kuwa rushwa ni adui wa haki. Mamant’ilie anashindwa kupiga hatua
katika biashara yake ya kuuza chakula kwa sababu mgambo wa jiji walichukua
rushwa kwake kila siku. Faida yote ya Mamant’ilie inaishia mikononi mwa mgambo
na kumfanya ashindwe hata kusomesha watoto wake. Katika jamii yetu rushwa ipo,
bila kutoa rushwa huwezi kuhudumiwa, ni vyema vyombo vilivyopewa dhamana ya
kupambana na rushwa vikaongeza bidii ili kutokomeza uovu huu.
Sambamba
na hayo kwa kutumia riwaya ya TAKADINI, kauli hii inathibitishwa kama
ifuatavyo,
Fasihi
inatufundisha kuwa walemavu wanaweza kufanya mambo makubwa na muhimu katika
jamii kama walivyo watu wengine. Takadini pamoja na ulemavu wake aliweza
kufanya mambo mengi kama kuimba, kupiga mbira, kutibu watu na mambo mengine
mengi yaliyowashangaza watu waliowanyanyasa walemavu. Katika jamii yetu walemavu
wakipewa nafasi wanaweza kufanya mambo makubwa ya kuisaidia jamii. Pia wapo
walemavu wa ngozi ambao wanajishughulisha na shughuli mbalimbali kwa mafanikio
makubwa.
Fasihi
inatufundisha kuwa baadhi ya mila zimepitwa na wakati na hazifai kuendelea
kutumiwa. Miongoni mwa mila hizo ni zile zinazowataka walemavu wauawe. Takadini
ananusurika kuuawa lakini ujasiri wa mama yake unamsaidia. Jamii yetu imekuwa
na Tamaduni ya kuwaficha na kuwatenga watu wenye ulemavu, pia watu wenye
ulemavu wa ngozi wanakabiliwa na wimbi kubwa la mauji ambapo wauaji wanaamini
kuwa viungo vyao vinaweza kutumika kuwapatia utajiri. Hii ni imani potofu na
inabidi kutokomezwa kwa nguvu zote.
Fasihi
inatufundisha kuwa ndoa ni makubaliano ya watu wawili na haipaswi kuingiliwa na
mtu yeyote. Takadini anapendana na Shingai lakini wazazi wake Shingai
hawakubaliani na jambo hilo kwa sababu tu Takadini ni mlemavu wa ngozi. Pamoja
na pingamizi la wazazi Shingai anashikilia msimamo wake na wanapata mtoto
asiyekuwa na ulemavu wa aina yoyote. Wapo wazazi katika jamii yetu ambao
wamejaribu kuingilia mahusiano ya watoto wao na kuwaharibia maisha. Jambo hili
halikubaliki na ni kinyume na haki za binadamu.
Hivyo ndivyo
fasihi ilivyotumika kufundisha maisha kwa jamii. Mafundisho yaliyopo katika
fasihi yana umuhimu mkubwa katika ujenzi wa jamii mpya hivyo ni vyema kwa
wanajamii kuyafuata mafunzo hayo yenye mchango chanya.
Mfano
wa pili; swali la tamthiliya Swali la necta mwaka 2008 “Waandishi wengi
huandika kazi zao kwa lengo la kutoa ujumbe katika jamii”. Kwa kutumia
tamthiliya mbili (2) zilizoorodheshwa, thibitisha ukweli wa kauli hii.
JIBU
Ujumbe ni
funzo linalopatikana katika kazi ya fasihi. Ni kweli kabisa kuwa waandishi
wengi huandika kazi zao kwa lengo la kutoa ujumbe katika jamii. Kauli hii
inaweza kuthibitishwa kwa kutumia tamthiliya mbili, KILIO CHETU chao Medical
Aid Foundation na NGOSWE – PENZI KITOVU CHA UZEMBE kilichoandikwa na Edwin
Semzaba. Kwa kuanza na tamthiliya ya KILIO
CHETU inathibitishwa kuwa,
Mwandishi
anatoa ujumbe kuwa elimu ya ujinsia na mahusiano itolewe kwa watoto. Elimu hii
ni muhimu na inahitajika sana kuwakomboa watoto dhidi ya maambukizi ya virusi
vya UKIMWI. Tunamuona Suzi na Joti wakiwa hawana elimu ya jinsia na mahusino,
madhara yake ni kwamba, Joti anamwambukiza Suzi virusi vya UKIMWI pia
anamsababishia mimba. Pengine wangepewa elimu wasingepatwa na matatizo. Hata
katika jamii yetu elimu ya jinsia na mahusiano inahitajika ili iweze kuwaokoa
watoto dhidi ya maradhi. Ni vyema kuachana na ukale unaopiga vita elimu hii.
Mwandishi
anatoa ujumbe kuwa sayansi na teknolojia itumiwe kwa uangalifu kwani inaweza
kuwaathiri watoto. Joti, Chogo, Jumbe na Mwarami wanaangalia mikanda ya ngono
bila kuwa na hofu yoyote. Uangaliaji wa picha hizi unawafanya watamani
kuyafanya yale wayaonayo. Suala hili linahatarisha elimu na maisha yao. Hata
katika jamii yetu ni vyema watoto wakasimamiwa na wazazi wao katika vipindi
waangaliavyo katika televisheni. Watoto waangalie vipindi ambavyo vitawasaidia
kukua katika maadili mema.
Mwandishi
anatoa ujumbe kuwa asiyefunzwa na mamaye hufunzwa na ulimwengu. Joti ni mhusika
ambaye hakufunzwa vyema na wazazi wake badala yake anaadabishwa na dunia.
Kulingana na mienendo mibaya ya kijana huyu kama vile kutembea na wanawake
waliomzidi umri, anaambukizwa virusi vya UKIMWI na kupelekea kifo chake. Katika
jamii yetu watoto aina ya Joti wapo, hivyo wazazi wanatakiwa wawafunze vyema
watoto wao, elimu pekee wanayotakiwa kuwapa ni elimu ya jinsia na mahusiano.
Sambamba
na hayo, kwa kutumia tamthiliya ya NGOSWE – PENZI KITOVU CHA UZEMBE, kauli hii
inathibitishwa,
Mwandishi
anatoa ujumbe kuwa tusichanganye mapenzi na kazi. Ngoswe anamtamani mtoto wa
Mzee Mitomingi na kusahau kazi ya kuhesabu watu iliyompeleka, anajaribu
kutoroka na Mazoea lakini anasahau makaratasi ya sensa ambayo yanachomwa na
Mzee Mitomingi na kuifanya hesabu iharibike. Katika jamii yetu watu
wanaoendekeza mapenzi badala ya kazi wapo, suala hili linarudisha nyuma
maendeleo kwani kazi hazifanyiki kwa ufanisi. Ni vyema kutofautisha kati ya
muda wa kazi na muda wa mapenzi.
Mwandishi
anatoa ujumbe kuwa hasira ni hasara. Mzee Mitomingi anafanya maamuzi akiwa na
hasira. Maamuzi ya kuyachoma moto makaratasi ya sensa yanasababisha hasara
kubwa kwa serikali na wananchi, kwani lengo la watu kuhesabiwa ni kuirahisishia
serikali upangaji wa maendeleo katika nchi yake. Katika jamii yetu hasara kubwa
zimetokea kwa sababu ya watu waliojaribu kufanya maamuzi wakiwa na hasira, watu
wengi wamejikuta wakiua kwa sababu ya hasira na hasira zilipokwisha wakaanza
kujuta. Kama mtu anahasira, basi asifanye maamuzi yoyote.
Mwandishi
anatoa ujumbe kuwa suala la malezi lihusishe wazazi wote wawili. Katika jamii
ya Mitomingi, wanawake ndio wanapewa jukumu la malezi ya watoto wao. Mazoea
anapotoroshwa na Ngoswe Mzee Mitomingi anawalaumu wake zake kwa kushindwa
kuchukua hatua. Katika jamii yetu suala hili lipo kwa kiasi kikubwa. Mama peke
yake kuachiwa mzigo wa malezi kumesababisha jamii yetu iwe na watoto ambao
hawana maadili sawasawa. Ni vyema suala la malezi likahusisha wazazi wote
wawili kama wapo.
Waandishi
huandika kazi zao kwa lengo la kuifundisha jamii. Ni jukumu la wanajamii
kuyafuata mafunzo hayo ili kusaidia katika ukombozi wa jamii. Ni dhahiri kuwa
mengi yasemwayo na waandishi huwa na malengo ya kuikomboa jami
Maoni
Chapisha Maoni